Mabingwa wa soka Tanzania Bara Yanga leo wanaianza kampeni ya kuwania tiketi ya kutinga hatua ya makundi ya michuano ya ligi ya mabingwa barani Afrika (CAFCL) pale watakapoikabili CFFA ya Madagascar.
Mchezo huo wa mkondo wa mkondo wa kwanza utapigwa saa tisa Alasiri kwenye uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.
Ni dakika 90 kati ya 180 za kuwania tiketi ya kufuzu hatua ya makundi Wananchi wakiisaka rekodi ya kutinga hatua hiyo kwa msimu wa nne mfululizo.
Ni wazi hautakuwa mchezo mwepesi kila timu ikiwa na lengo la kutinga makundi lakini kwa Yanga unaweza kusema hawatakuwa na utetezi endapo watashindwa kusonga mbele hasa kwa kuzingatia wamepata nafasi ya mechi zote mbili kupigwa nyumbani.
Aidha Yanga imepata muda wa kutosha kujiandaa na mchezo huo baada ya kupoteza mchezo uliopita dhidi ya watani zao Simba ukiwa mchezo wa ligi kuu ya NBC.
Kocha Manqoba Mngqithi amepata wiki moja ya kukiandaa kikosi chake kuelekea mchezo huo.
Matarajio ya mashabiki wa Yanga ni kuona timu yao ikiibuka na ushindi mnono leo na kujiweka kwenye nafasi nzuri ya kutinga hatua ya makundi pale timu hizo zitakaporudiana tena uwanja wa Azam Complex Oktoba 21.