Yanga leo imetoa onyo kwa timu nyingine zinazoshiriki ligi kuu ya NBC ikiifumua Mashujaa Fc mabao 6-0 katika mchezo uliopigwa uwanja wa KMC Complex.
Wananchi walitawala mchezo huo tangu dakika ya kwanza lilikuwa ni suala la mabao mangapi Yanga ingefunga katika mchezo huo.
Mohamed Damaro aliyefungua kalamu ya mabao mapema tu kwenye dakika ya 7 akimaliza kwa kichwa mpira ulioparazwa na Dickson Job.
Pacome Zouzoua na Duke Abuya wakaongeza mawili kabla ya mapumziko na kuwapeleka Wananchi mapumziko wakiwa kifua mbele kwa mabao 3-0.
Kipindi cha pili Yanga iliendeleza ilipoishia kipindi cha kwanza na kuongeza mabao mengine matatu kupitia kwa Prince Dube, Mudathir Yahya na Laurindo Dilson 'Depu' aliyeingia kipindi cha pili.
Depu alimalizia mpira uliotemwa na mlinda lango Erick Johora baada ya shuti la Allan Okello kupitia mpira wa adhabu.
Sio kufunga tu, Depu pia alitoa pasi ya bao lililofungwa na Mudathir Yahya.
Ni ushindi mnono unaoipeleka Yanga kileleni mwa msimamo wa ligi. Ni salamu kwa wapinzani, wajipangeeee..




