Yanga imetakata uwanja wa KMC Complex leo ikiibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Fountain Gate katika mwendelezo wa ligi kuu ya NBC.
Ulikuwa mchezo uliotawaliwa na mbinu zaidi huku Yanga ikianza taratibu lakini ilikwenda mapumziko ikiwa mbele kwa bao 1-0 likifungwa na Prince Dube kupitia mkwaju wa penati baada ya mlinzi wa Fountain Gate kunawa mpira ndani ya eneo la hatari.
Kipindi cha pili Fountain Gate walionekana kuimarika zaidi huku Yanga ikiendelea kusaka bao la pili na alikuwa ni Pacome Zouzoua aliyeingia kipindi cha pili akifunga bao la pili akimalizia pasi ya Duke Abuya.
Unaweza kusema Wananchi hawakuwa katika kasi yao iliyoonekana katika mechi chache zilizopita pengine ni kutokana na uchovu wa mechi mfululizo na safari kutoka Algeria.
Aidha mkufunzi wa Yanga Pedro Concalves amesema hali ya jua kali iliathiri kwa kiasi kikubwa ufanisi wa wachezaji wake.
Amesema watakuwa na muda wa kupumzika na kujiimarisha zaidi kuelekea mchezo unaofuata dhidi ya Coastal Union siku ya Jumapili.