Klabu ya Simba SC imesema itaweka skrini kubwa (big screen) katika Viwanja vya Mwembe Yanga, Temeke, Dar es Salaam, ili mashabiki wake waweze kutazama mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya FC 15 de Agosto ya Guinea ya Ikweta.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Jumatano katika Uwanja wa Uhuru, Dar es Salaam, kuanzia saa 9 alasiri, bila mashabiki uwanjani, baada ya wapinzani wao kuamua mchezo huo uchezwe bila watazamaji.
Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC, Ahmed Ally, amesema maandalizi ya kuweka big screen yanalenga kuwapa Wanamsimbazi nafasi ya kuushuhudia mchezo huo na kuendelea kuipa timu yao sapoti licha ya kutokuwepo uwanjani.
Aidha, Ahmed amesisitiza kuwa sharti kwa mashabiki watakaofika Mwembe Yanga kutazama mchezo huo ni kuvaa jezi mpya ya Simba SC.
Vilevile, amewataka mashabiki wa Simba kuwa makini na wito wowote kutoka kwa wapinzani wao kuhusu kwenda uwanjani, akisisitiza umuhimu wa kufuata maelekezo ya klabu yao kuhusu mchezo huo.
Kupitia mpango huo, Simba inalenga kuwakutanisha mashabiki wake katika eneo moja ili kushuhudia mchezo huo wa kimataifa na kuendeleza hamasa ya kuisapoti timu yao katika kampeni ya Ligi ya Mabingwa Afrika.