Kikosi cha Simba SC kimeingia siku ya pili ya maandalizi yake katika kambi ya siku 10 inayoendelea jijini Polokwane, Afrika Kusini, huku Kocha Mkuu Steve Barker akiendelea kukifanyia kazi kikosi chake kwa maandalizi ya mchezo wa ligi kuu dhidi ya Yanga pamoja na mechi nyingine zitakazoendelea baada ya mapumziko ya kalenda ya FIFA.
Barker ameendelea na programu yake ya mazoezi huku akipokea nyota zaidi wanaowasili kambini kuungana na wenzao na kuanza maandalizi kwa pamoja.
Miongoni mwa wachezaji waliowasili Polokwane na kuanza kushiriki mazoezi ni winga Elie Mpanzu, beki Ismail Toure na kinda Bashir Kibaila, ambao hawakuwa sehemu ya wachezaji waliowasili mapema Afrika Kusini.
Kambi hiyo inatajwa kuwa ya kimkakati zaidi kwa maandalizi ya Simba, benchi la ufundi likitumia muda huo kuwafanyia tathmini wachezaji, kuboresha mifumo ya uchezaji na kuwaweka tayari kimwili na kiufundi.
Simba imeingia kwenye maandalizi hayo ikitumia kipindi hiki ambacho ligi imesimama ili kujiimarisha ziadi wakihitaji utulivu kuweka sawa mipango yao.
Unaweza kusema msimu huu Wekundu wa Msimbazi wamedhamiria kupeleka ubingwa Msimbazi kwani wanachuana jino kwa jino na watani zao Yanga ambapo timu zote zimeanza vyema msimu zikishinda mechi zote sita.
Mchezo baina ya timu hizo utakaopigwa Oktoba 10 utatoa taswira na mwelekeo wa msimu kwa timu zote mbili.