Vinara wa ligi kuu ya Vodacom Yanga, leo wako jijini Tanga ambapo majira ya saa kumi Alasiri watashuka kunako dimba la Mkwakwani kuwakabili wenyeji wao Coastal Union
Huu ni mchezo wa mzunguuko wa 22, Wananchi wakihitaji alama zote tatu ili waendelee kujichimbia kileleni mwa msimamo wa ligi
Hata hivyo wanacheza katika uwanja ambao umekuwa mgumu kwao kuondoka na alama zote tatu
Mara ya mwisho Yanga kushinda mchezo wa ligi katika uwanja wa Mkwakwani ni mwaka 2015
Hivyo wachezaji wanafahamu ugumu wa mchezo huo lakini ili uweze kuwa bingwa lazima ushinde mechi za aina hii
Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amesema kikosi chake kiko tayari kwa mchezo huo licha ya kuwakosa baadhi ya wachezaji kutokana na sababu mbalimbali
Nyota wanaokosekana leo ni Saido Ntibazonkiza, Mapinduzi Balama, Ditram Nchimbi na Adeyum Saleh ambao ni majeruhi
Carlinhos yeye anatumikia adhabu ya kukosa mechi tatu
Ili kuhakikisha wanaondoka na alama zote tatu, viongozi waandamizi wa Yanga wakiongozwa na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Mashindano Injinia Hersi Said, wako jijini Tanga kuhakikisha Wagosi wa Kaya 'wanakufa' hapo Mkwakwani
Yanga inatarajiwa kupata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wake na wale wa African Sports, mtani wa jadi wa Coastal Union wakati mashabiki wa Simba wanatarajiwa kuiunga mkono Coastal Union
Jiji la Tanga leo litasimama muda wa jioni kupisha mchezo ambao umevuta hisia za mashabiki ndani ya jiji hilo