Mwenyekiti wa kamati ya Maadili Kachele Mwita amesema Kamati yake haikumjadili tena mchezaji Bernard Morrison kwa kuwa hawajapelekewa mafaili yake na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF)
Ikumbukwe baada ya mchezaji huyo kutangazwa kuwa yuko huru na kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji, alipelekwa Kamati ya Maadili kwa kosa la kusaini mkataba na klabu ya Simba na wakati shauri lake na Yanga likiwa bado linasikilizwa
Morrison aliwahi kuitwa kwenye Kamati ya Maadili, hakuhudhuria na hakuna hatua iliyochukuliwa dhidi yake
Ikumbukwe mapema Yanga ilipeleka malalamiko TFF ikiituhumu klabu ya Simba kumhadaa Morrison aweze kujiunga nao wakati wakifahamu ana mkataba na Yanga
Kwa kinywa chake mwenyewe, Morrison alithibitisha kuhongwa dola 5,000 na aliyemuita kuwa Wakala wa klabu ya Simba ambaye alitumwa ampatie fedha hizo alizodai zimetoka kwa 'Mo'
Malalamiko haya ya Yanga hayakuwahi kusikilizwa na TFF mpaka sasa
Sasa juzi TFF ikatangaza kumfungia Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli kwa miaka mitatu akidaiwa kugoma kulipa faini ya Tsh Milioni tano kutokana na makosa aliyodaiwa kuyafanya wakati wa shauri la Morrison
Inashangaza Kamati ya Maadili imeweza kuhukumu makosa yaliyofanywa na Bumbuli lakini wakasahau kuwa hata Morrison mwenyewe alikuwa na kesi za kujibu mbele ya Kamati hiyo na hata walipomuita mara ya kwanza hakuhudhuria
Aidha Kaimu Katibu Mkuu wa Yanga Haji Mfikirwa amethibitisha kuwa hata fedha ambazo Morrison alipaswa kuzirudisha Yanga bado hajakamilisha kuzirudisha
TFF wenyewe wamejitetea kuwa walisitisha kumjadili Morrison baada ya Yanga kupeleka shauri lake Mahakama ya Kimataifa ya Usuluhishi wa Michezo (CAS)
Hii ni aibu kubwa kwa Shirikisho la Soka kuwa na maamuzi ambayo hayavitendei usawa vilabu vyote wanavyovisimamia
Pamoja na kuwa Serikali haziruhusiwi kuingilia vyama vya michezo, lakini kuna haja kwa Serikali yetu kupitia kwa Baraza la Michezo la Taifa (BMT) waimulike TFF kubaini madudu yanayoendelea