Kipindi cha usajili wa dirisha dogo, timu kadhaa zilijitokeza kumuwania mshambuliaji wa Yanga Waziri Junior ambaye amekosa nafasi katika kikosi cha kwanza
Hata hivyo Waziri amefichua kuwa kocha Cedric Kaze aligoma kumuondoa mchezaji huyo katika kikosi chake
Waziri aliyeshika nafasi ya pili katika orodha ya wafungaji bora msimu uliopita, msimu huu amefunga bao moja tu kwenye ligi
Alitua Yanga akiwa na matumaini makubwa lakini ushindani wa namba uliochangiwa na ubora wa kikosi cha Yanga umepelekea mwamba huyo wa CCM Kirumba kushindwa kuonyesha makali yake
"Kama mchezaji sifurahii kuwa sipati nafasi mara kwa mara kwani kazi yangu mimi ni kucheza mpira. Lakini naheshimu uamuzi wa Mwalimu kwani yeye ndiye anayeamua nani aanze katika mchezo upi"
"Ni kweli nilitamani kuondoka dirisha dogo baada ya timu kadhaa kuonyesha kunihitaji lakini kocha (Kaze) hakutaka niondoke akinieleza bado ananihitaji"
"Hivyo nitaendelea kujituma na kupigania nafasi naamini wakati wangu utafika nitacheza," alisema Waziri
Baada ya usajili wa Fiston Abdul Razak, safu ya ushambuliaji sasa inaundwa na wachezaji wanne Michael Sarpong, Waziri Junior, Yacoub Songne na Fiston. Ushindani wa namba unatarajiwa kuwa mkali zaidi