Mlinda lango wa Yanga Farouk Shikhalo amesema ataendelea kufanya vizuri ili kumpa mwalimu wakati mgumu kuamua nani amuanzishe katika kikosi chake cha kwanza
Shikhalo alikaa langoni jana kwenye mchezo wa kombe la Mapinduzi dhidi ya Jamhuri Fc, akiokoa Yanga isipoteze mchezo kwenye dakika za majeruhi
"Nampongeza mwenzangu (Metacha) kwa kufanya vizuri kwani sote lengo letu ni moja. Namshukuru Mwalimu kwa kunipa nafasi leo, naahidi nitaendelea kufanya vizuri kila ninapopata nafasi kama hii"
"Mimi sina presha yoyote ninapokuwa nje, jukumu langu ni kuhakikisha nafanya vizuri nikipewa nafasi ili presha ibaki kwa Mwalimu anapoamua nani aanze," alisema Shikhalo
Akizungumzia matokeo ya mchezo huo uliomalizika kwa suluhu ya bila kufungana, Shikhalo alisema lengo lao lilikuwa kuondoka na ushindi lakini anawapongeza Jamhuri Fc kwani waliwapa changamoto
"Wajua hakuna timu ndogo kwenye haya mashindano, sisi tulikuja kwa lengo la kushinda na wenzetu nao ni hivyohivyo. Kipindi cha kwanza hatukucheza vizuri sana, tulikuwa tukijaribu mfumo mpya lakini kipindi cha pili tulirejea tukiwa imara. Sio matokeo tuliyoyataka lakini tumekubaliana nayo, tunajipanga ili tuweze kufanya vizuri kwenye mchezo unaofuata"
"Muhimu ni kuwa tumejifunza kitu kwa mchezo wa leo na nina imani tutafanya vizuri zaidi katika mchezo unaofuata"