Kocha Mkuu wa Yanga Cedric Kaze amesema anatarajia mchezo wenye ushindani mkali dhidi ya Azam Fc ambao utapigwa baadae leo uwanja wa Azam Complex
Hata hivyo amesema vijana wake wako tayari kuelekea mchezo huo lengo likiwa kupata ushindi
Aidha Kaze amesema katika mchezo huo nyota wake wawili Abdulaziz Makama na Haruna Niyonzima watakosekana
Niyonzima bado hajarejea kutoka Rwanda, hivi karibuni akikumbwa na mkasa wa kupata ajali
Makame alipewa ruhusu kurejea kwao Zanzibar kushughulikia matatizo ya kifamilia
"Tunategemea mchezo utakuwa mgumu Azam ni timu bora na tumelingana pointi kwahiyo kila timu ingependa kupata ushindi ili kukaa kileleni mwa msimamo"
"Sisi tumejipanga vizuri na lengo letu ni kupata pointi zote tatu. Tutawakosa wachezaji wawili Haruna Niyonzima ambaye ni majeruhi pamoja na Abdulaziz Makame mwenye matatizo ya kifamilia," alisema Kaze
Mechi hii ya kukata na shoka itapigwa kuanzia saa moja usiku. Ni mchezo mwingine ambao utapima dhamira ya Yanga ya kuwania ubingwa msimu huu
Kwani ili uweze kuwa bingwa unapaswa kupata matokeo katika michezo ya aina hii
Hivyo wananchi leo wataingia uwanjani wakifahamu, bila ya alama tatu, watawapa fursa watani zao Simba ambao mechi zao za raundi ya 12 na 13 zimepigwa kalenda kutokana na ushiriki wao wa michuano ya ligi ya mabingwa