Matokeo ya sare ya bao 1-1 dhidi ya Simba leo hayakufurahiwa na mashabiki wa Yanga lakini muhimu zaidi ni kwa mabingwa hao wa kihistoria kuwazima watani zao Simba ambao kabla ya mchezo walitamba kuibuka na ushindi mnono
Yanga ilikuwa bora sana kwenye kipindi cha kwanza, mbinu ya mashambulizi ya kushitukiza iliyotumiwa na Cedric Kaze ilikuwa na mafanikio kwani hata bao lilitokana na shambulizi lililofanywa kupitia Tuisila Kisinda
Kipindi cha pili Kaze alibadili mfumo, aliweka wachezaji wengi nyuma ya mpira ili kudhibiti presha ya wachezaji wa Simba waliokuwa wakihaha kusaka bao la kusawazisha
Aidha kuumia kwa Lamine Moro kulipunguza umakini kwenye safu ya ulinzi ya Yanga hivyo kutoa mwanya kwa Simba kuweza kusawazisha kupitia mpira wa kona uliojazwa kimiani na Onyango
Kaze alifahamu mchezo hautakuwa mwepesi, mpango wake ilikuwa kuhakikisha anapata matokeo kwenye kipindi cha kwanza na kipindi cha pili akitumia mfumo wa kujilinda zaidi na kushambulia kwa kushitukiza
Ukiwa mchezo wake wa kwanza wa dabi, sio matokeo mabaya sana kwa kocha Kaze hasa ukiangalia muda aliokaa timu
Simba wameendelea na kunufaika na kikosi chao ambacho kimekuwa pamoja kwa karibu misimu mitatu sasa
Yanga bado imebaki kuwa timu pekee ambayo haijafungwa msimu huu, hii ni hatua muhimu sana katika kampeni ya kuwania ubingwa wa ligi kuu msimu huu
Baada ya mchezo huo, ligi imesimama kwa wiki mbili kupisha michuano ya Kimataifa kuwania kufuzu fainali za Afcon 2021
Benchi la ufundi litakuwa na takribani wiki mbili za kuimarisha timu hasa kwa wachezaji ambao hawatakuwa na majukumu ya timu za Taifa
Mchezo utakaofuata utapigwa Novemba 22 dhidi ya Azam Fc