Ni alama nyingine tatu kibindoni kwa Yanga baada ya kuwachapa watoza ushuru wa Kinondoni KMC kwa kuwafunga mabao 2-1 katika mchezo uliopigwa uwanja wa CCM Kirumba
Mbinu za kocha Cedric Kaze ambaye leo alianza na washambuliaji wawili, zimekuwa na mafanikio kwa Yanga kwani mabao yote mawili yametokana na juhudi za washambuliaji Michael Sarpong na Waziri Junior
Ulikuwa ni mchezo uiojaa ufundi na ushindani kutoka kila upande, KMC ndio walioanza kufunga bao la kuongoza kwenye dakika ya 27 kupitia kwa Hassan Kabunda

Kabunda alifunga bao hilo kwa shuti akiwa nje kidogo ya 18 baada ya walinzi wa Yanga kuchelewa kumdhibiti, alikokota mpira kwa hatua chache kabla ya kufunga bao hilo
Kuingia kwa bao hilo kuliiamsha Yanga ambayo iliongeza kasi ya mashambulizi na juhudi zilizaa matunda kwenye dakika ya 41, Tuisila Kisinda akiisawazishia Yanga kupitia mkwaju wa penati
Ni baada ya Sarpong kufanyiwa madhambi ndani ya eneo la hatari

Kipindi cha pili Yanga iliendelea kulishambulia lango la KMC na hakika ilikuwa siku muhimu sana kwa Waziri Junior aliyefungua akaunti yake ya mabao msimu huu akiunga kwa kichwa kona ya Farid Mussa kwenye dakika ya 61
Kaze amemwamini Junior tangu alipotua na leo ameipa thamani imani hiyo aliyopewa kwani bao lake limeihakikishia Yanga ushindi muhimu
Matokeo hayo yanamfanya Kaze aendeleze rekodi ya ushindi kwa asilimia 100 baada ya kushinda michezo yote miwili huku kikosi chake kikiendelea kuimarika
Aidha, ushindi huo umeendelea kuiweka Yanga katika nafasi ya pili ikifikisha alama 19 sasa wakiwa nyuma ya Azam Fc kwa tofauti ya alama mbili
Mchezo unaofuata ni dhidi ya Biashara United, utapigwa Oktoba 30 kule Musoma