Aliyewahi kuwa kiungo mahiri wa Yanga Athumani Idd Chuji amesema kiungo Mcongomani Mukoko Tomombe amempitisha kuwa mrithi wake halisi ndani ya kikosi cha Yanga
Mukoko ameanza vyema maisha yake ndani ya Yanga akifunga jumla ya mabao matano, mawili kwenye ligi na matatu katika mechi za kirafiki
Bao la dakika ya 70 alilofunga katika mchezo dhidi ya Polisi Tanzania Alhamisi iliyopita, liliihakikishia Yanga ushindi muhimu uliowapandisha nafasi ya pili
Chuji ameonyesha kumkubali Mukoko na anaamini atafika mbali ndani ya kikosi cha Yanga
"Safi sana kijana, tutaongea kesho (leo), nakuachia kila kitu, pambana, unakuja na uko vizuri," aliandika Chuji kwenye ukurasa wake wa mtandao wa kijamii
Pamoja na uhodari wake wa kucheza vyema nafasi ya kiungo na hata beki wa kati, Chuji alikuwa mahiri sana katika kupiga zile pasi za kuhamisha uwanja

Pasi yake moja ilitosha kutengeneza mashambulizi ya haraka kupitia mawinga kina Saimon Msuva
Mukoko amemkumbusha Chuji enzi zake, kwani awapo dimbani hachoki na wakati wote anapambana kuhakikisha timu inapata matokeo
Chuji alitangaza kustaafu mwanzoni mwa msimu huu baada ya kucheza soka la ushindani kwa zaidi ya miaka 15