Kocha wa zamani wa Manchester United, Sir Alex Fegurson aliwahi kusema kuwa safu bora ya ushambuliaji itakupa ushindi katika mechi lakini safu bora ya ulinzi itakupa ubingwa
Kauli hii inadhihirisha umuhimu wa kuwa na safu bora ya ulinzi linapokuja suala la kushinda ubingwa
Msimu huu safu ya ushambuliaji ya Yanga imeanza kwa mwendo wa kinyonga, pengine ni kutokana na ugeni wa wachezaji katika eneo hilo
Hata hivyo safu ya ulinzi imeiweka timu salama, ikiwa inashika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi wakiwa na alama 13 sawa na mabingwa watetezi Simba ambao wanatamba kuwa na safu bora ya ushambuliaji
Msimu uliopita, eneo la ulinzi lilikuwa tatizo kubwa kwa Yanga, ilikuwa sio rahisi sana kwa Yanga kuondoka na 'cleansheet'
Msimu huu mpaka sasa Yanga ina cleansheet nne kwenye ligi, ukuta wa Yanga uliruhusu bao pekee katika mchezo wake wa kwanza msimu huu dhidi ya Tanzania Prisons
Tangu wakati huo hakuna bao walilofungwa tena iwe kwenye ligi na hata michezo ya kirafiki
Ni kazi kubwa inayofanywa na manahodha Lamine Moro na Bakari Nondo Mwamnyeto ambao ndio wanasimama mbele ya mlinda lango Metacha Mnata
Hawa wanasaidiana na walinzi wa pembeni Kibwana Shomari, Yassin Mustafa, Deus Kaseke na Adeyum Saleh kwa nyakati tofauti bila ya kuwasahau viungo zawadi Mauya, Tonombe Mukoko na Feisal Salum ambao kwa wastani wameshirikiana katika mechi kadhaa
Kocha Cedric Kaze ana kazi moja tu, kuhakikisha anatengeneza muunganiko pale mbele ili kuzalisha mabao mengi
Huku kwenye ulinzi hapaswi kuwa na wasiwasi kwani tayari anao watu wa kumuhakikishia ubingwa