Miongoni mwa wachezaji ambao watanufaika na ujio wa kocha Cedric Kaze kwenye kikosi cha Yanga ni kiungo Carlos Carmo 'Carlinhos'
Chini ya Kaze, Carlinhos mwenye uhodari wa kupiga pasi na mipira ya adhabu, atakuwa na uhakika wa kutumika katika nafasi yake
Wakati Yanga ikinolewa na Zlatko Krmpotic, fundi huyo kutoka Angola alikuwa akitumika kama winga, nafasi ambayo sio asili yake
Kaze alimsifu Carlinhos kuwa na vitu vingi mguuni kwake ambavyo anaamini vitainufaisha Yanga
Kwa mfumo wa Kaze wa kumiliki mpira, huenda tukamshuhudia Carlinhos akitumika katika nafasi anazomudu uwanjani, ambazo ni namba nane na kumi
Hata hivyo Carlinhos atapaswa kujituma kwelikweli ili kuhakikisha anadumu kwenye kikosi cha Kaze kwani Mrundi huyo hana masihara na amesisitiza kuwa anahitaji timu ya wachezaji 11 na sio watu 11 uwanjani
Miongoni mwa maeneo ambayo Carlinhos anapaswa kujiimarisha ni katika ukabaji hasa timu inapokuwa haina mpira
Kocha Msaidizi wa Yanga Juma Mwambusi amedokeza kuwa wanaendelea kumuimarisha Carlinhos ambaye alikaa nje kwa takribani miezi sita kabla ya kutua Yanga
Ligi Kuu ya Angola ilisimama kwa muda mrefu baada ya kuzuka janga la corona mapema mwaka huu