Ligi Kuu ya Vodacom msimu wa 2020/21 inazidi kuchanja mbuga ambapo michezo ya raundi ya nne itaanza kupigwa kesho Ijumaa
Siku ya Ijumaa mechi mbili zinatarajiwa kupigwa mkoani Mbeya na kule Kagera
Kagera Sugar iliyotoka kuchapwa bao 1-0 na Yanga kwenye uwanja wake wa nyumbani, itashuka tena katika dimba lake kumenyana na KMC
KMC wameanza vyema msimu baada ya kushinda mechi zote tatu na kukaa kileleni mwa msimamo wa ligi
Mbeya City nao watakuwa nyumbani kuumana na Namungo Fc. Mbeya City mpaka sasa wana alama 0 kwani wamepigwa mechi zote tatu walizocheza
Michezo mingine mitatu itapigwa siku ya Jumamosi ambapo Polisi Tanzania watakuwa nyumbani wakiumana na Dodoma Jiji
Simba itakuwa uwanja wa Mkapa kuumana na Gwambina Fc wakati Tanzania Prisons watashuka uwanja wa Nelson Mandela mkoani Rukwa kuikaribisha Azam FC
Jumapili mabingwa wa kihistoria Yanga watakuwa ugenini kule mkoani Morogoro wakiwa wageni wa Mtibwa Sugar katika mchezo utakaopigwa uwanja wa Jamhuri
Siku hiyohiyo, Ruvu Shooting watacheza na Biashara United na Mwadui Fc wakicheza na Ihefu Fc
Mechi za raundi ya nne zitakamilika Jumatatu kwa Wagosi wa Kaya Coastal Union kuumana na JKT Tanzania mkoani Tanga