Moja ya wachezaji ambao Wanayanga wanajivunia usajili wake ni huyu Farid Mussa ambaye ametokea moja kwa moja kule nchini Hispania kujiunga na Yanga
Farid anaangaliwa kwa jicho la kipekee na mashabiki akitarajiwa kuwa mmoja wa wachezaji watakaoibeba Yanga msimu unaoanza mwezi ujao
Ni mchezaji aliyepata uzoefu mkubwa huko Hispania, ameiva kwelikweli angalia kazi anayoifanya anapokuwa kwenye kikosi cha timu ya Taifa
Farid hakuja Yanga kwa bahati mbaya, ni mchezaji mwenye malengo makubwa, akiwa na imani anaweza kuyafanikisha malengo hayo ndani ya Yanga

Muda sio mrefu Yanga itakuwa daraja kwa wachezaji wengi kwenda nje ya nchi hasa kule Hispania. Ushirikiano wao wa miaka mitatu na La Liga pamoja na klabu ya Sevilla, utafungua fursa kibao kwa wachezaji wa Yanga hasa wale vijana
Mwenyewe Farid amesema anafahamu kitu gani mashabiki wa Yanga wamekikosa kwa takribani misimu mitatu hivyo ujio wake ni nkuhakikisha wanatimiza ndoto ya kushinda ubingwa
"Nafahamu nini mashabiki na wapenzi wa klabu wanachotaka . Nipo hapa kuwatumikia, kufunga magoli na kuhakikisha tunapata ushindi, Kutwaa ubingwa ndio ndoto yangu kubwa na kwa klabu yangu," amesema
Wanayanga wanasubiri kumshuhudia Farid pamoja na nyota wengine wapya kwenye kilele cha wiki ya Mwananchi Jumapili ijayo