Msimu uliomalizika nahodha msaidizi Juma Abdul alijihakikishia nafasi ya kudumu kwenye safu ya ulinzi upande wa kulia katika kikosi cha Yanga
Dogo Paulo Godfrey 'Boxer' alisumbuliwa na majeraha yaliyopelekea apoteze nafasi yake kwenye kikosi na baadae shindwa kupenya katika timu ya Luc Eymael, kocha aliyetimuliwa na Yanga hivi karibuni
Katika usajili wake, inaelezwa Yanga inaweza kuongeza mlinzi mwingine wa kulia, na kama hilo likitokea, ni wazi hatma ya Boxer itakuwa shakani
Kumekuwa na tetesi kuwa Yanga inataka kumrejesha Hassan Ramadhani Kessy ambaye amerejea nchini baada ya kumaliza mkataba wake na Nkana Fc kule Zambia
Hivi karibuni Kessy alionekana viunga vya Jangwani, kukiwa na uwezekano mkubwa kwake kupewa mkataba
Wanachofanya viongozi wa Yanga katika usajili wa kuelekea msimu ujao ni kutengeneza ushindani kwenye kila nafasi ili wachezaji wawajibike
Kessy na Abdul walicheza pamoja kikosi cha George Lwandamina, ni Kessy aliyekuwa na nafasi mbele ya Abdul ingawa nyota hao walikuwa wakipokelezana katika baadhi ya mechi
Lakini pia pengine Yanga bado inahitaji kuwa na Boxer, kwani ni mchezaji aliyeonyesha ukomavu wakati wa Mwinyi Zahera ambaye alimpandisha timu ya wakubwa kutoka kikosi cha vijana
Anachohitaji ni kupata nafasi ya kucheza mara kwa mara ili kurejesha makali yake
Umri wake pia bado ni mdogo, hivyo ni mchezaji ambaye anaweza kuja kumbadili Juma Abdul miaka michache ijayo