Pamoja na changamoto nyingi msimu huu, Yanga imefunga msimu 'kibabe' kwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Lipuli Fc na kujihakikishia kumaliza katika nafasi ya pili
Msimu wa 2019-20, ulijaa machungu mengi kwa mashabiki, msimu huu unapaswa kuwa somo kwa mabosi wa Yanga kuhakikisha hawarejei makosa yaliyopelekea timu isiweze kufikia malengo na matarajio ya wengi
Jambo kubwa ambalo kila shabiki anataka kuona ni umakini katika usajili wa wachezaji
Msimu huu uliomalizika Yanga ilisajili wachezaji wapya wanaofika 22, ni kutokana na makosa yaliyofanywa kwenye usajili wa dirisha kubwa ambapo mabingwa hao wa kihistoria kwa usaidizi wa GSM, walilazimika kufanya usajili mwingine mwezi Januari wakati wa dirisha dogo
Lakini pia kulikuwa na mabadiliko ya benchi la ufundi katikati ya msimu, jambo ambalo kwa kiasi kikubwa liliathiri muunganiko wa timu
Jambo muhimu zaidi ambalo mabosi wa Yanga wanapaswa kulizingatia ni muda wa maandalizi ya msimu mpya
Msimu huu Yanga haikuwa na maandalizi mazuri. Timu iliweka kambi mkoani Morogoro tena ikinolewa na kocha msaidizi kwa muda mwingi
Pengine michuano ya Afcon 2019 ilichangia kukosekana kwa kocha Mwinyi Zahera, lakini Mcongomani huyo angeweza kurudi mapema kwani timu yake ilitolewa mapema tu kwenye raundi ya kwanza
Kambi nzuri, muda wa kutosha kufanya maandalizi, ni mambo ya msingi ambayo yanapaswa kuzingatiwa katika maandalizi yajayo
Wanayanga kila mmoja atakuwa makini kufuatilia yanayoendelea pale Jangwani kwani kwa hakika hakuna shabiki ambaye atakuwa tayari kuendelea 'kuugulia' msimu ujao