Nahodha wa Yanga Papy Tshishimbi amesema afya yake imeimarika na yuko tayari kushuka dimbani kwenye mchezo wa nusu fainali kombe la FA dhidi ya Simba ambao utapigwa Jumapili Julai 12 katika uwanja wa Taifa
Tshishimbi amekosekana kwenye kikosi cha Yanga tangu ligi iliporejea baada ya mapumziko ya corona kutokana na majeraha
Mcongomani huyo alianza mazoezi mepesi wiki iliyopita lakini hakujumuishwa katika safari ya Yanga kanda ya ziwa akikosa michezo dhidi ya Biashara United na Kagera Sugar
"Binafsi najisikia nimepona lakini bado nasubiri ruhusa ya madaktari kuweza kurejea rasmi uwanjani. Natamani niicheze mechi hiyo (dhidi ya Simba) nitawaomba makocha wangu wanipe hata dakika 40 zitatosha kuisaidia timu yangu," amesema Tshishimbi
Tshishimbi ameendelea kujifua jijini Dar es salaam wakati wenzie wakiwa Bukoba ambako jana walicheza dhidi ya Kagera Sugar na kuibuka na ushindi wa bao 1-0
Ana nafasi ndogo ya kushiriki mchezo huo ambao utahitaji kila mchezaji kuwa na utimamu wa mwili na akili ili kuhakikisha wanaivusha Yanga hatua ya fainali ya michuano hiyo