Mshambuliaji Ditram Nchimbi jana alihusika kwenye ushindi wa mabao 3-2 ambao Yanga iliupata dhidi ya Ndanda Fc ukiwa ni mchezo wa ligi kuu
Nchimbi ndiye 'aliyepika' bao la kwanza lililowekwa kimiani na Deus Kaseke
Kuelekea mchezo wa robo fainali kombe la FA dhidi ya Kagera Sugar ambao utapigwa keshokutwa Jumanne katika uwanja wa Taifa, Nchimbi amesema ushindi waliopata mchezo dhidi ya Ndanda, umewaongezea mzuka kuelekea mchezo huo
Nchimbi ambaye alitua Yanga usajili wa dirisha dogo akitokea klabu ya Polisi Tanzania akitua kwa mkopo kutoka Azam Fc, amewataka mashabiki wa mabingwa hao wa kihistoria kujitokeza kwa wingi Jumanne kuwaunga mkono ili waweze kushinda mchezo huo
"Matokeo tuliyopata mechi dhidi ya Ndanda yametuongezea mzuka, lengo letu ni kuona tunashinda mchezo dhidi ya Kagera Sugar ili tuweze kutinga nusu fainali ya FA," alisema Nchimbi
Aidha nyota huyo amesema mchezo wa Kagera Sugar ni wa mtoano hivyo watacheza tofauti na walivyocheza mechi zilizopita ili kuhakikisha wanapata matokeo yatakayowapeleka hatua inayofuata
Yanga itakumbana na Kagera Sugar ikiwa na kumbukumbu ya kufungwa mabao 3-0 katika mchezo wa ligi kuu uliopigwa mapema mwaka huu
Nchimbi amesema bado anakikumbuka kipigo hicho kwani ulikuwa mchezo wake wa kwanza tangu aliposajiliwa na Yanga