Kocha Msaidizi wa Yanga Charles Mkwasa amewahakikishia Mashabiki wa Yanga kuwa kikosi chao kiko tayari kwa mchezo wa ligi kuu dhidi ya Mwadui Fc ambao utapigwa uwanja wa CCM Karambare siku ya Jumamosi
Yanga inatarajiwa kusafiri kuelekea mkoani Shinyanga tayari kwa mchezo huo ambao utafungua ngwe ya mwisho ya msimu wa ligi kuu ya Vodacom ambao ulisimamishwa kutokana na ugonjwa wa corona
Baada ya kipigo cha mabao 3-0 kutoka kwa KMC kwenye mchezo wa kirafiki, baadhi ya mashabiki wameonyesha kukata tamaa hasa kutokana na kiwango duni kilichoonyeshwa na mabingwa hao wa kihistoria
Mkwasa amesema anaamini mazoezi ya mwisho wanayofanya kabla ya kuelekea Shinyanga, yatawasaidia kurekebisha makosa yao na watafanya vizuri
"Kufungwa ni matokeo ambayo hatukuyatarajia, lakini muhimu ni kuwa mchezo ule umetusaidia kubaini mapungufu yetu kabla ya mechi za ligi kuanza. Tutaendelea kujiimarisha na hakuna wasiwasi tutakuwa vizuri. Lengo letu ni kufanya vizuri mechi zote zilizobaki kwenye ligi na michuano ya kombe la FA," amesema Mkwasa
Mkwasa anaendelea kukiandaa kikosi cha Yanga kwa ajili ya mchezo dhidi ya Mwadui Fc wakati kocha Mkuu Luc Eymael alitarajiwa kuwasili Jumatano mchana
Uongozi wa Yanga umesema Eymael ataungana na timu mkoani Shinyanga
Β