Kiungo wa Mtibwa Sugar Abdulkarim Humud yuko tayari kuwatumikia mabingwa wa kihistoria Yanga huku akiweka wazi kuwa hayuko tayari kuichezea klabu ya Simba hata ikitokea imempa ofa nono
Nyota huyo ambaye amekuwa na msimu mzuri katika klabu ya Mtibwa Sugar, katika moja ya mahojiano yake amefunguka kuwa hana tatizo ikitokea amepewa ofa na Yanga lakini ofa ya Simba 'ataipotezea'
Humud amewahi kuzitumikia Simba na Azam Fc kabla ya kwenda nje ya nchi kusaka changamoto mpya
Kiungo huyo anatajwa kuwa miongoni mwa wachezaji wazawa ambao kocha Luc Eymael amewatupia jicho na kutamani kufanya nao kazi
Tetesi za Humud kutua Yanga zilipata kasi wakati wa sakata la kiungo Papy Tshishimbi alipokuwa akisuasua kusaini mkataba mpya
Hata hivyo baada ya Tshishimbi kusaini, hakuna taarifa kuhusu Humud ingawa Eymael ameagiza aletewe kiungo mwingine mkabaji ambaye atampa changamoto Tshishimbi
Wakati nyota wa Rayon Sports, Ally Niyonzima akitajwa zaidi kukaribia kutua Jangwani, Humud anaweza kuwa mbadala kama dili la nyota huyo wa timu ya Taifa ya Rwanda litakwama