Kocha Mkuu wa Yanga Luc Eymael amesema anaangalia utaratibu wa kuianza safari ya kurejea nchini kuungana na timu yake kumalizia ngwe iliyobaki
Eymael aliyeondoka nchini mwishoni mwa mwezi March kwenda kufunga ndoa, ameshindwa kurejea kutokana na vikwazo vya safari za Kimataifa katika nchi nyingi kutokana na janga la corona
Mbelgiji huyo amesema huenda safari yake itakuwa na mzunguuko mrefu lakini muhimu ni kwake kuwahi kurejea kabla ligi haijaanza
"Najipanga kurejea Tanzania, ipo changamoto ya usafiri, pengine naweza kuwa na mzunguuko mrefu. Jambo la muhimu ni kurejea kwa wakati kuungana na timu," amesema
Aongeza dozi ya mazoezi
Katika hatua nyingine, Eymael amewatumia wachezaji wake program nyingine ya mazoezi ambayo wanapaswa kuianza leo Jumatatu
Katika jitihada za kukiweka kikosi chake sawa tayari kwa kucheza mechi mfululizo, Eymael amesema anaamini mazoezi hayo yatawaongezea wachezaji pumzi na stamina
Mbelgiji huyo amesema amempa majukumu maalum nahodha Papy Tshishimbi kuhakikisha program hiyo inawafikia wachezaji wote lakini pia kufuatilia wanafanya mazoezi hayo
Β