Beki wa zamani wa Yanga mkongwe Keneth Pius Mkapa amesikia mpango wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kutaka kutilia mkazo wachezaji wa kigeni wanaokuja kucheza hapa nchi wawe wanacheza timu za Mataifa wanayotoka
Mkapa amesema mpango huo ni mzuri kwani utawezesha vilabu kuwa na wachezaji wa kigeni wenye sifa sahihi, hata hivyo amesema kwa Tanzania unaweza kukwama kutokana na gharama za wachezaji hao kuwa juu
Mkapa amesema haamini kama vilabu vya Tanzania vitaweza kusajili wachezaji wanaocheza timu za Taifa ambazo viwango vyao vya soka viko juu kuliko Tanzania
"Kwa kweli suala la wachezaji wetu wa kigeni kuwa wanacheza timu zao za taifa litakuwa gumu kwani sidhani kama kuna klabu Tanzania inaweza kusajili mchezaji anayecheza timu ya taifa ya Ghana,Mali ama Cameroon"
"Nadhani ni vyema TFF waweke utaratibu ambao angalau utaweka masharti mchezaji awe amepita timu ya taifa ya vijana itatosha," amesema
Ukiachana na mjadala wa idadi ya nyota wa kigeni ambao ulitawala vyombo vya habari siku za karibuni, Bodi ya Ligi pia ilidokeza kuwa kuanzia msimu ujao wachezaji wa kigeni watakaotakiwa kusajiliwa na vilabu hapa nchini wanapaswa kuwa wanacheza timu za Mataifa yao