Mwishoni mwa msimu uliopita mashabiki wa Yanga walipigwa na butwaa baada ya kumshuhudia kupitia mitandao mshambuliaji wao tegemeo Heritier Makambo kuonekana akiwa ndani ya uzi wa Horoya Ac huku taarifa zikibainisha kuwa alikuwa amesaini mkatana wa miaka mitatu kuwatumikia mabingwa hao wa Guinea
Mchakato wa kuuzwa Makambo inaelezwa ulisimamiwa na aliyekuwa kocha mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera ambaye aliambatana nae Guinea kukamilisha dili hilo liliofanyika kimyakimya
Aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uchumi na Fedha Shija Richard amefichua kuwa dau la mauzo ya mchezaji huyo lilikuwa zaidi ya fedha waliyopewa klabu ya Yanga
Yanga ilipokea kitita cha Tsh Milioni 170 lakini baadae walibaini kuwa Makambo aliuzwa Tsh Milioni 250
"Dili la Makambo awali klabu haikuhusishwa, tulistukia tu yuko na kocha Mwinyi Zahera ambaye aliomba kwenda kwao likizo baadae ndipo wakaonekana na Makambo," Shija amenukuliwa na gazeti la Mwanaspoti
Shija ambaye alijiuzulu nyadhifa zake zote ndani ya klabu ya Yanga hivi karibuni, amesema kuwa baadae Zahera aliwapigia simuΒ na kueleza kuwa Horoya AC iko tayari kutoa Tsh Milioni 170 muda huohuo ili imnunue Makambo
Zahera aliwaambia viongozi wa Yanga wanapaswa kuamua wakati huo kama hawako tayari kumuuza amrudishe
"Kocha alifanya vile akijua hali halisi ya kiuchumi tulikaa na kujadiliana hilo kilikuwa ni kipindi ambacho tulipswa kusajili na klabu haikuwa na fedha," alisema
Hata hivyo mwaka jana Zahera alikanusha tetesi kuwa alikuwa Wakala wa Makambo ambapo alijitetea kuwa uongozi wa Yanga ulimruhusu aongozane na Makambo Guinea kukamilisha dili hilo kwa kuwa nchi hiyo wanaongea Kifaransa lugha ambayo yeye huzungumza