Kiungo mshambuliaji wa Yanga Bernard Morrison amefichua kuwa viongozi wa klabu ya Simba walinza kumfuatilia mapema wakitaka kumpa mkataba wa awali ili ajiunge na timu hiyo mwezi Juni
Morrison ambaye wiki iliyopita aliongeza mkataba wa miaka miwili kuendelea kuitumikia Yanga, mabingwa wa kihistoria, amesema mara ya kwanza viongozi wa Simba kumfuata ilikuwa kabla ya mchezo wa watani wa jadi uliopigwa March 08
"Unajuwa wengi wanadhani Simba wameanza kunifuata karibuni, lakini ukweli ni kwamba walianza kabla ya mchezo tuliocheza nao March 08," amesema Morrison
"Walifahamu mimi nilikuwa na mkataba wa miezi sita, wakatumia mwanya huo kunishawishi ili nisaini mkataba wa muda mrefu kwao"
"Mimi sikuwa na cha kusema zaidi ya kumuachia Wakala wangu ambaye waliendelea kuwasiliana nae. Lakini mwisho wa siku nimeamua kuendelea kubaki Yanga"
Raia huyo wa Ghana amekuwa na mwanzo mzuri kunako klabu ya Yanga akiwa amefunga mabao manne na kutoa pasi tano za mabao kwenye mashindano yote
Pia alikuwa akiwaniwa na vilabu kadhaa kutoka Afrika Kusini