Mwezi uliopita, mlinda mlango wa klabu ya Yanga, Ramadhan Kabwili alitoa tuhuma nzito kuwa aliwahi kufuatwa na uongozi wa klabu ya Simba wakitaka atafute kadi ili asicheze mchezo wa watani na wampatie gari aina ya IST
Baada ya TFF kutangaza kuanza kwa uchunguzi wa tukio hilo, uongozi wa Yanga ulizungumza na Kabwili ili kukusanya taarifa sahihi za tukio hilo
Afisa Habari wa Yanga Hassan Bumbuli amesema tayari suala hilo liko mikononi mwa Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU)
"Suala la Kabwili halipo mikononi mwetu tena, limeshafika TAKUKURU na ndio maana mimi kama mimi nikiwa mwakilishi wa Yanga siwezi lisemea "
"Taarifa kuhusu lilipofikia nadhani TAKUKURU ndio wanaweza kuwa na majibu," amesema
Kabwili alitoa tuhuma hizo alipokuwa akihojiwa katika kipindi cha Kipenga Xtra cha East Africa Radio, ambapo alibainisha jaribio hilo la kuhongwa lilitokea wakati Yanga ikiwa na kocha Mwinyi Zahera.
Alisema kuwa siku hiyo Yanga ilikuwa inaelekea kucheza na JKT Tanzania na yeye alikuwa na kadi mbili za njano, hivyo Simba walimfuata na kumuambia kuwa atafute kadi moja ya njano ili akose mchezo uliokuwa unafuatia wa watani wa jadi huku wakimuahidi kumpa IST mpya, wakiamini kuwa angekaa Klaus Kindoki golini wangemfunga kirahisi.