Mashabiki wa Yanga kwa sasa tunapita kwenye nyakati ngumu kutokana na mwenendo usioridhisha wa timu yetu
Ukweli ni kwamba Wanayanga hatukuzoea haya yanayojiri sasa kwani kwa miaka mingi Yanga tumekuwa na kawaida ya kufurahi tu
Mataji 27 ya ligi kuu ni kielelezo tosha kuwa furaha imejiri Jangwani mara nyingi kuliko mahali pengine
Lakini huu ni msimu wa tatu sasa mambo hayajakaa sawa
Misimu miwili iliyopita Wanayanga tunaweza kuwa na sababu kwa nini timu yetu haikufanya vizuri. Ni kutokana na changamoto za kiuchumi
Lakini msimu huu kila mmoja alikuwa na matumaini makubwa kuwa timu itafanya vizuri
Wanayanga wenyewe tumeshiriki kwenye kampeni mbalimbali za kuichangia timu yetu na baadae GSM kuingia kuongeza nguvu
Aidha ujio wa GSM ni kama uliongeza hamasa zaidi kwani waliongeza uhakika wa maisha ya wachezaji hasa suala la wachezaji kulipwa stahiki zao kwa wakati
Lakini sare nne mfululizo zimetukatisha tamaa mashabiki, kwani hatuoni kama timu yatu itafikia malengo yake
Wakati mwingine ndivyo matokeo ya mpira yanavyokuwa
Hapa jambo la msingi ni kwetu Wanayanga kutulia, kuendelea kuiunga mkono timu yatu kwani nyakati hizi zitapita tu
Hiki ni kipindi cha mpito ambacho kila timu bila ya kujali ukubwa wake, itapita
Kwa wale wanaofuatilia ligi kuu ya Uingereza wanaweza kuona kinachowatokea Manchester United
Hawa ni miamba wa soka la Uingereza, wakiwa na mataji mengi kuliko timu zote
Lakini kwa misimu kadhaa wamepoteza makali yao, wanafanya juhudi ili kurejesha furaha ya mashabiki wao
Bingwa wa kweli lazima apite katika majaribu haya ambayo kwa njia moja au nyingine, yatazidi kumkomaza
Tunachohitaji Yanga sasa ni kuwa watulivu kwani juhudi za kuimarisha timu zinafanyika, sote tunaona
Nyakati za furaha haziko mbali, muhimu tujiepushe kuanzisha migogoro ambayo inatufanya tuanze upya kila mara