Wakati mashabiki wengi wakionekana kukata tamaa na ubingwa wa ligi kuu msimu huu, kocha msaidizi wa Yanga Charles Mkwasa amesema bado ni mapema sana kukata tamaa
Yanga ilipoteza matumaini baada ya kupata sare tatu mfululizo, matokeo yaliyowafanya waambulie alama tatu kati ya tisa
Mabingwa hao wa kihistoria wana deni la alama 19 dhidi ya vinara wa ligi Simba lakini pia wakiwa na michezo miwili ya viporo
Mkwasa amesema kutokana na ushindani ulivyo mkali hasa baada ya kuingia duru ya pili, lolote linaweza kutokea
"Ligi bado ni ngumu sana, umeona kila timu inatoa upinzani mkali. Muhimu kwetu ni kuendelea kupambana ili kuhakikisha tunapata matokeo kwenye michezo yetu"
"Suala la ubingwa bado ni mapema sana, hakuna timu ambayo imejihakikishia ubingwa sasa kwani mechi bado ni nyingi. Kwenye mpira wa miguu lolote linawezekana," amesema
Yanga imekusanya alama 40, imebaki na mechi 17 ambazo KAMA watashinda zote watafikisha jumla ya alama 91
Msimu uliopita Simba ilitwaa ubingwa ikikusanya alama 92 wakati Yanga ikimaliza nafasi ya pili ikiwa na alama 86
Yanga inahitaji kukusanya alama zaidi ya 45 kutoka michezo 17 iliyobaki na wakati huo huo ikiomba mambo yaende kombo kwa watani zao Simba