Nahodha wa Yanga, Papy Tshishimbi amesema aina ya soka wanalocheza kwa sasa chini ya kocha wao mpya Luc Eymael linatoa nafasi ya kushambulia zaidi tofauti na awali.
Tshishimbi ameiongoza Yanga kuibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Mtibwa Sugar, alisema wakati wakiwa chini ya Mwinyi Zahera walikuwa wakicheza kwa kujilinda zaidi hasa katika michezo mikubwa huku wakitumia mipira mirefu kushambulia.
βKila kocha amekuwa na mbinu za namna yake. Zahera alikuwa bora kwa wakati wake, Eymael anapenda tucheze soka la kushambulia zaidi huku tukicheza pasi fupi fupi na kupiga ndefu penye ulazima wa kufanya hivyo,β alisema Tshishimbi.
Hata hivyo aina ya soka la Eymael, Tshishimbi alisema halijawachukua muda kulizoea pamoja na kuwa asilimia kubwa ya wachezaji ilikuwa imezoea soka la pasi ndefu.
βTulipata shida kidogo katika michezo miwili ya mwanzo ambayo tulicheza vizuri, lakini tukapoteza, baada ya hapo aina ya soka letu likawa linaendana na matokeo,β alisema.
Wakati akijiunga na Yanga, Eymael aliweka wazi aina yake ya soka huku akitoa ahadi kwa wapenzi na mashabiki wa timu hiyo kuwa watarajie soka safi na ushindi katika michezo mbalimbali.
Katika michezo mitano ambayo ameiongoza Yanga katika mashindano yote tangu akabidhiwe mikoba ya Zahera, Eymael ambaye ni raia wa Ubelgiji, ameifanya klabu hiyo kuibuka na ushindi katika michezo mitatu na kupoteza miwili.
Yanga ambao wapo nafasi ya tatu katika msimamo wa Ligi Kuu Bara wakiwa na pointi 31, kesho Jumatano watakuwa na kibarua kingine cha kucheza dhidi ya Lipuli FC.