Mshambuliaji wa timu ya Kagera Sugar, Yusuph Mhilu, amesema kitendo cha Kocha wa Taifa Stars, Etienne Ndayiragije, kumwita katika kikosi chake kutamsafishia njia ya kurejea katika klabu yake ya zamani ya Yanga.
Wiki iliyopita Ndayiragije alitangaza kikosi cha Tanzania Bara, Kilimanjaro Stars, kinachotarajiwa kuanza mazoezi leo kujiandaa na michuano ya Chalenji itakayoanza Desemba 7, mwaka huu, Uganda.
Mhilu ni miongoni mwa wachezaji waliojumuishwa kwenye kikosi hicho cha wachezaji 32
"Yanga ndio timu iliyoniibua katika soka hivyo siku zote naiheshima na kuithamini pia, niliondoka kwenda kwa mkopo Ndanda, baada ya kuonekana nimeshuka kiwango kipindi cha kocha Mwinyi Zahera," Mhilu ameliambia gazeti la Bingwa
"Kuitwa Kilimanjaro Stars kwangu ni jambo kubwa sana kwani naamini changamoto nitakazozipata huko zitaniongezea uwezo na kunipa nafasi ya kurudi kuitumikia Yanga ambayo imenilea na kunionesha njia katika soka"
Mhilu ni moja ya wachezaji waliopandishwa katika kikosi cha kwanza cha Yanga na kocha Hans van der Pluijm misimu mitatu iliyopota akitokea timu ya vijana, lakini msimu uliopita alijikuta akipelekwa Ndanda kwa mkopo, baada ya Zahera kudai ameshuka kiwango.