Baada ya kushindwa kufikia makubaliano na uongozi wa Yanga kuhusu malipo ya madai yake, beki Andrew Vicent 'Dante' amesema hatma yake itafahamika dirisha dogo la usajili litakapofunguliwa mwezi ujao
Tangu kuanza kwa msimu huu Dante 'alijiondoa' Yanga akishinikiza alipwe malimbikizo ya madai ya fedha za usajili zaidi ya Tsh Milioni 50
Beki huyo aliyeitumikia Yanga kwa mafanikio katika misimu mitatu, amesema hakuna mwafaka uliofikiwa kati yake na Yanga
"Nilianza kufanya mazungumzo vizuri na uongozi lakini badae tukashindwa kuelewana," amesema
"Ila bado naendelea kuwasikilizia hadi hapo dirisha dogo litakapofunguliwa ndio nitafahamu hatma yangu"
Yanga huenda ikalazimika kuvunja mkataba wa beki huyo kwani kwa zaidi ya miezi minne hayupo kazini
Aidha kwa upande wa Dante ni kama hayuko tayari kuendelea kucheza Yanga kwani uongozi wa timu hiyo ulikubali kumlipa fedha zake kwa awamu tatu lakini alikataa akitaka alipwe fedha zote kwa mkupuo
Nyota wengine waliokuwa na madai akiwemo nahodha Msaidizi Juma Abdul walikubali kupokea malipo yao kwa awamu na kuridhia kurejea kikosini