Kamati ya Ufundi ya klabu ya Yanga imekutana kujadili matengenezo ya uwanja wa Kaunda unaomilikiwa na klabu hiyo
Kamati hiyo ilitarajiwa kukutana jana jioni kuandaa mpango mkakati wa kukamilisha matengenezo hayo
Afisa habari wa Yanga Hassan Bumbuli alisema lengo lao ni kuhakikisha wanakamilisha angalau matengenezo ya sehemu ya kuchezea (pale ulipokuwepo uwanja wa zamani), ili timu ianze kufanya mazoezi
"Kamati ya Ufundi inakutana leo (jana), kuweka mkakati wa matengenezo ya uwanja, tutatoa taarifa rasmi kwa Wanayanga wote juu ya mkakati uliopo," alisema
Kumekuwa na zoezi la kumwaga kifusi ambalo limechukua muda mrefu kutokana na changamoto inayojitokeza kila mvua zinaponyesha
Lakini mpango uliopo ni kuhakikisha wanakamilisha kwa kuanzia sehemu ya kufanyia mazoezi wachezaji 'pitch' ingawa kwa baadae uwanja huo utajengwa kama ulivyokuwa zamani ili kuinufaisha klabu kwa mashabiki kulipa viingilio kushuhudia mazoezi lakini pia kuutumia kwenye michezo ya kirafiki