Ushindani waongezeka ligi kuu msimu huu

Shabiki NambaMoja By Shabiki NambaMoja
β€’
11 Nov 2019
Ushindani waongezeka ligi kuu msimu huu

Wakati mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu zikiwa zimesimama kwa muda kupisha kalenda ya kimataifa, hali imekuwa ni vuta nikuvute, timu nyingi zikionekana kuimarika zaidi tofauti na misimu kadhaa iliyopita.

Tumeshuhudia misimu iliyopita tukiona hadi kufikia wakati huu timu za Simba, Yanga, Azam, Mtibwa Sugar zikifuatana juu, lakini hali imekuwa tofauti kabisa kwa msimu huu, timu zisizotarajiwa ndizo zinamfukuza bingwa mtetezi kileleni, tena kwa tofauti ya pointi ndogo.

Mpaka kufikia raundi ya 11, misimu kadhaa iliyopita ilishuhudia timu zikigawana makundi matatu, zinazopigania kutwaa ubingwa, kutafuta pointi za kufanya zisishuke daraja na pia zinazopigana kufa na kupona ili zisiteremke.

Msimu huu timu zote kuanzia juu na kushuka chini hazijapishana sana pointi, hivyo kufanya kinyang'anyiro cha kuwania ubingwa wa msimu 2019/20 kuonekana kuwa kigumu.

Inawezekana kabisa msimu huu ligi imekuwa ngumu kwa sababu timu nne za juu huenda zote au tatu zikashiriki michuano ya kimataifa mwakani, Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho, huku timu sita zikiteremka daraja.

Ufafanuzi ni kwamba timu itakayoshika nafasi ya nne, inaweza kucheza Kombe la Shirikisho kama timu tatu za juu moja wapo itakuwa bingwa wa Kombe la FA.

Huko chini ni kwamba timu nne zitashuka daraja moja kwa moja na nyingine mbili zitacheza 'play off', na timu za Daraja la Kwanza Tanzania Bara, hivyo zinaweza nazo zisirudi hata moja.

Msimu huu hakuna timu yenye uhakika wa kushinda hata ikicheza nyumbani kwake. Timu inayojiandaa vema imekuwa ikipata ushindi hata ugenini.

Simba ambayo mpaka sasa inaongoza ligi ikiwa na pointi 22, ikicheza mechi tisa, iko kwenye wakati mgumu kwani chini yake kuna Kagera Sugar ambayo imefikisha pointi 20, mbili tu nyuma ya vinara hao, ikiwa imecheza mechi 10.

Ni Kagera Sugar ambao ilikuwa "almanusura" msimu huu icheze Daraja la Kwanza, kwani ilirejea Ligi Kuu kwa kucheza 'play' off' na kuifunga Pamba ya Mwanza na kupata tiketi ya kurejea Ligi Kuu tena, lakini sasa iko katika nafasi ya pili na tena ikifanya vema zaidi kwenye viwanja vya ugenini.

Prisons ambayo msimu uliopita haikuwa vizuri, msimu huu imejizatiti kwani pamoja na kukamata nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu kwa kujikusanyia pointi 19 katika michezo 11 iliyocheza, lakini hadi sasa ndio timu pekee haijapoteza mechi yoyote ile.

Lipuli ya Iringa, iliyotetemesha msimu uliopita, inaonekana labda msimu huu haitokuwa vizuri kutokana na kuondoka kwa kocha wake Selemani Matola na baadhi ya wachezaji akiwano, William Lucian 'Gallas' aliyekwenda Polisi Tanzania na Miraji Athumani aliyetua kwa mabingwa watetezi, lakini makali yake yameongezeka na inakamata nafasi ya nne kwa pointi 18, ikiwa tayari imeshacheza mechi 10.

Ingizo jipya kwenye Ligi Kuu msimu huu, Namungo FC inakamata nafasi ya tano ikiwa na pointi 16 kwa michezo 10 iliyocheza, huku Mtibwa Sugar, timu ambayo miaka kadhaa nyuma kwenye mechi za mwanzo ilikuwa ikitetemesha iko kwenye nafasi ya sita kwa pointi 15, Ruvu Shooting ikiwa kwenye nafasi ya saba kwa pointi hizo hizo 15.

Alliance, timu iliyopanda msimu uliopita na kuanza kwa kusuasua kabla ya kuzinduka mwishoni, msimu huu imeanza na moto, kwani mpaka sasa inakamata nafasi ya nane, ikiwa na pointi 14.

Katika hali inayoonyesha kuwa msimu huu hakuna lelemama, timu zilizozoea kukaa juu kama Azam FC inakamata nafasi ya 10 kwa kuwa na pointi 13, ikicheza michezo saba, Yanga ikiwa kwenye nafasi ya 15 kwa pointi 10, yenyewe ikicheza mechi tano.

Baadhi ya timu ambazo msimu uliopita zilikuwa moto wa kuotea mbali, lakini bado zinaonekana hazijaamka vizuri ni Mbao FC iliyo kwenye nafasi ya tisa kwa pointi 14, JKT Tanzania nafasi ya 12, ikiwa na pointi 12, KMC nafasi ya 16 kwa pointi nane, Mbeya City nafasi ya 18, ikiwa na pointi nane, Ndanda FC nafasi ya 19 ikiwa na pointi zake saba, na Singida United ambayo inaburuza mkia ikiwa na pointi nne.

Imeandikwa na Adam Fungamwango, kwa hisani ya Nipashe

ADVERTISE HERE

Yanga SC Stories

Aziz Ki atunukiwa tuzo ya kukuza vipaji
Aziz Ki atunukiwa tuzo ya kukuza vipaji
20m ago
READ MORE β†’
Baada ya Manqoba nani anafuata?
Baada ya Manqoba nani anafuata?
28m ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Alhamisi, Oktoba 29 2026
Magazeti ya leo Alhamisi, Oktoba 29 2026
3h ago
READ MORE β†’
Kundi la Yanga kama msimu uliopita tu
Kundi la Yanga kama msimu uliopita tu
18h ago
READ MORE β†’
Yanga yatupwa kundi B CAFCL
Yanga yatupwa kundi B CAFCL
19h ago
READ MORE β†’
Mzize ndio ameanza msimu hivyo
Mzize ndio ameanza msimu hivyo
22h ago
READ MORE β†’
Timu zinazoweza kukutana na Yanga makundi CAFCL
Timu zinazoweza kukutana na Yanga makundi CAFCL
23h ago
READ MORE β†’
Dladla alia na umaliziaji Yanga licha ya ushindi dhidi ya Mashujaa FC
Dladla alia na umaliziaji Yanga licha ya ushindi dhidi ya Mashujaa FC
1d ago
READ MORE β†’
Highlights: Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
Highlights: Yanga 2-1 Mashujaa Fc, NBC PL (FT)
1d ago
READ MORE β†’
Magazeti ya leo Jumatano, Oktoba 28 2026
Magazeti ya leo Jumatano, Oktoba 28 2026
1d ago
READ MORE β†’