Kuna uwezekano mkubwa Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga Charles Boniface Mkwasa ataiongoza timu hiyo mpaka dirisha dogo la usajili na kisha kocha mpya kuchukua majukumu baada ya dirisha hilo kufungwa
Inaaminika kuwa tayari Yanga imeshampata Kocha Mkuu lakini pengine amehitaji muda ili kukifanyia tathmini kikosi ili kuweza kufanya maboresho wakati wa dirisha dogo la usajili
Kwa mechi ambazo Yanga tayari imecheza msimu huu, kuna maeneo ambayo ni dhahiri yameonyesha mapungufu
Beki wa kushoto
Baada ya Yanga kushindwa kumbakisha Gadiel Michael ambaye aligoma kusaini mkataba dakika za majeruhi, viongozi walimsajili Muharami Issa 'Marcelo' wakimtoa Singida United kwa msaada wa Dk Mwigulu Nchemba
Hata hivyo 'Marcelo' ameshindwa kufikia matarajio hivyo muda mwingi Ally Mtoni ambaye kwa asili ni beki wa kati, kutumika katika nafasi hiyo
Hivyo ni dhahiri Yanga inahitaji kusajili beki mwingine wa kushoto ambaye atasaidiana na Marcelo huku Sonso akirudishwa safu ya ulinzi wa kati
Inaelezwa Yanga tayari imemalizana na Rayon Sports kuhusu usajili wa Erick Rutanga ambaye anatajwa kuelekea Jangwani dirisha dogo
Kiungo mchezeshaji
Pamoja na kuwa na viungo wengi, Yanga imekosa kiungo mbunifu ambaye angeweza kurahisisha kazi ya washambuliaji pale mbele
Mohammed Issa 'Banka' alianza msimu vizuri lakini baadae alipata majeraha ambayo yamemuweka nje kwa zaidi ya wiki nane sasa
Papy Tshishimbi, Abdulaziz Makame na Feisal Salum wote wanaonekana kuwa viungo wazuri, lakini hawakuwa na athari katika kutengeneza nafasi za mabao
Mapinduzi Balama hakuwa akitumika zaidi kwenye nafasi ya kiungo na kocha Mwinyi Zahera pengine Mkwasa anaweza akamtumia katika nafasi hiyo
Kiungo wa zamani wa Yanga Haruna Niyonzima anatajwa kuwa tayari amemalizana na viongozi wa timu hiyo na anasubiriwa kutua wakati wa dirisha dogo
Niyonzima ni aina ya viungo wabunifu, kama Yanga itafanikiwa kumrejesha, hakuna shaka ataongeza ubora wa safu hiyo
Mshambuliaji
Washambuliaji wote waliosajiliwa na kocha Mwinyi Zahera wameshindwa kuonyesha makali
Yawezekana mfumo uliokuwa ukitumiwa na Zahera uliwapa wakati mgumu lakini hilo litaweza kufahamika wakati huu ambao timu iko chini ya Mkwasa
Lakini vyovyote itakavyokuwa, Yanga inahitaji mshambuliaji mwingine mwenye uwezo wa juu zaidi ambaye atasaidiana na David Molinga na Juma Balinya
Kwa anavyoonekana Sadney sio mshambuliaji wa kati, anaweza kuwa bora zaidi kama akitokea pembeni
Michael Sarpong mshambuliaji wa Kimataifa wa Ghana mwenye umri wa miaka 23 akitokea klabu ya Rayon Sports anatajwa kuwaniwa na mabingwa hao wa kihistoria
Zahera hakuwa na vipaumbele vya usajili
Pengine moja ya mambo ambayo yamemponza Zahera na hadi kupelekea kupoteza kibarua chake Yanga ni pamoja na usajili wake kutokuwa na uwiano sawa na matakwa ya timu
Changamoto zinazoonekana kwenye kikosi cha Yanga sasa angeweza kuzitatua kama usajili wake angeufanya kwa umakini
Yanga ilisajili walinzi wa kati wanne ambao ni Ally Ally, Ally Mtoni, Lamine Moro na Mustafa Suleyman wakati huo ikiwa na Kelvin Yondani na Andrew Vicent
Pengine alipaswa kuongeza walinzi wawili tu wa kati, nafasi nyingine angesajili mlinzi mwingine wa pembeni
Washambuliaji aliowasajili pengine ni bora angembakisha Amissi Tambwe kisha kuongeza mshambuliaji mwingine kuchukua nafasi ya Heritier Makambo ambaye uuzwaji wake uligubikwa na utata
Kutokana na mapungufu yaliyopo Yanga italazimika kuingia gharama kufanya usajili mwingine ili kuhakikisha kikosi kinakuwa imara ili kuweza kushindana na Simba katika kuwania ubingwa wa ligi kuu