Baadhi ya mashabiki Yanga leo wamemshushia lawama kocha Mwinyi Zahera kuwa amekuwa chanzo cha timu kutofanya vizuri dhidi ya Pyramids Fc
Tukio la kusikitisha limejitokeza CCM Kirumba baada ya mchezo kumaliza ambapo mashabiki wasiokuwa waungwana walimshushia matusi Zahera huku wengine wakimrushia mawe na chupa
Kimsingi makocha ndio wabebaji wakuu wa lawama pale timu inapokuwa haifanyi vizuri, huwa wanaajiliwa ili wafukuzwe
Hivyo ni sawa kwa Zahera kulaumiwa baada ya timu kufungwa leo
Lakini wakati mwingine ni vyema kuangalia mazingira ambayo yanapelekea timu kufungwa
Yatakuwa makosa makubwa kwa Wanayanga kuangalia upande mmoja tu kuwa tumefungwa na hivyo lazima kocha aondoke
Pamoja na makosa ya hapa na pale ya kiufundi, Yanga leo imecheza na timu bora lazima ukweli usemwe
Kwa mchezaji mmoja mmoja, wachezaji wa Pyramids Fc walionyesha utofauti mkubwa baina yao na wale wa Yanga
Tofauti ya uwekezaji baina ya timu hizi mbili umedhihirishwa na uwezo wa wachezaji
Hawa Pyramids wameonekana ni timu iliyokamilika. Ushindi wao pengine walistahili, kwa sababu walikuwa bora
Lakini pia Yanga tunataka mafanikio ya haraka bila ya kupitia utaratibu unaotakikana
Soka linahitaji uwekezaji sio siasa. Kwa kiasi kikubwa ujio wa Zahera amesaidia kuleta mabadiliko ya fikra za baadhi ya Wanayanga
Yeye ndiye aliyekuja na wazo la kuwashirikisha mashabiki na wanachama kuichangia timu yao ili usajili ufanyike
Fedha zilipatikana za kusajilii lakini ukweli ni kwamba sio kwa kiasi ambacho wengi wanafikiria
Yanga haikuwa na uwezo wa kusajili wachezaji wa viwango vya juu kwani haikuwa na fedha za kutosha na hata sasa bado haina fedha
Leo hii kuna wachezaji kama Andrew Vicent wamegoma kujiunga kambini sababu wana madai na viongozi wamebainisha wazi kuwa hawana fedha za kuwalipa kwa mkupuo
Hivyo ni wazi, pamoja na Zahera kupewa jukumu la kusajili lakini bado fungu la usajili alilopewa lilimbana hivyo kutafuta wachezaji wa kiwango kinachoendana na fedha iliyopo
Uongozi wa Yanga unaweza kufanya uamuzi wa kumuondoa Zahera hata leo lakini sidhani kama kuna jambo litabadilika kwa haraka
Kama ni lazima Yanga kubadili kocha, basi itapaswa kocha mpya aandaliwe mazingira ya kumfanya afanikiwe ikiwa ni pamoja na kuandaliwa fungu la kutosha kufanya usajili wakati wa dirisha dogo
Swali ni kwamba Yanga ina fedha za kuyafanya hayo? jibu ni kwamba kwa sasa haina
Hivyo ni dhahiri kocha mpya hatakuwa na mabadiliko makubwa ya kikosi, nae atahitaji muda kuijenga timu yake
Swali, Je mashabiki watavumilia wakati huo ambao huyo kocha mpya atakuwa akijenga timu yake hasa ikitokea timu haipati matokeo?
Hapa ndipo fukuza fukuza ya makocha itakapoanzia