Yanga ilikumbwa na changamoto kubwa za kiuchumi baada ya mfadhili wake na aliyekuwa Mwenyekiti Yusufu Manji kukumbwa na matatizo
Manji aliilemaza Yanga, kwani alifanya kila jambo yeye mwenyewe, alipoondoka timu ikaingiaa katika dimbwi la umasikini
Katika misimu miwili iliyopita, tumeishuhudia Yanga ikikabiliwa na ukata uliopelekea kurudisha nyuma maendeleo ya timu
Yanga ina madeni makubwa kwani ukiachilia mbali kudaiwa na wachezaji, wana madeni kutoka taasisi za kibenki na hata watu binafsi
Uongozi mpya ulioingia madarakani mwezi May, una kazi kubwa ya kumaliza changamoto hiyo
Hivi karibuni suala la deni la beki Andrew Vicent limezungumzwa sana kwenye vyombo vya habari, huku uongozi ukishushiwa lawama kwa kushindwa kumlipa beki huyo ambaye amegoma mpaka alipwe fedha zote zinazofikia Mil 40
Yanga ilipendekeza kumlipa kwa awamu tatu kutokana na hali yake ya kiuchumi ilivyo, aligoma
Lakini si yeye peke yake mwenye madai Yanga, wachezaji waliotumikia timu hiyo katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, wengi wana madai, wengine wamehama kujiunga na timu nyingine huku wakiwa na madai
Wakati wakihangaika kulipa madeni hayo, uongozi unajitahidi kuwalipa stahiki za wachezaji waliopo ili kuepuka kutengeneza madeni mapya
Hili wapo wanaochukulia kama upendeleo lakini ukweli ni kwamba hiyo ndio njia pekee kumaliza madeni. Kwani kama wataruhusu kutengeneza madeni mapya hawataweza kumaliza changamoto hiyo
Yanga inahitaji kuongeza kipato chake ili kumaliza madeni, jitihada zinaonekana pengine baada ya muda watafanikiwa kuyamaliza