Safu ya ushambuliaji ya Yanga bado haijaweza kuwapa furaha mashabiki wake kutokana na uhaba wa mabao
Sadney Urikhob, Juma Balinya na Patrick Sibomana waliaminiwa mapema na kocha Mwinyi Zahera kuiongoza safu hiyo
Hata hivyo zaidi ya kufunga mabao ya mipira ya adhabu, bado washambuliaji hao hawajafanya kile wanachotaka mashabiki
Mganda Juma Balinya alitarajiwa kuiongoza safu hiyo kutokana na umahiri wake katika kuzifumania nyavu
Balinya alitua Yanga akitokea klabu ya Polisi Fc ya Uganda ambapo msimu uliopita aliibuka mfungaji bora wa ligi ya nchi hiyo akifunga mabao 21
Tangu atue Yanga, amefunga bao moja tu kwenye mechi za mashindano kupitia mpira wa adhabu kwenye mechi ya ligi ya mabingwa dhidi ya Township Rollers
Zahera amesema mshambuliaji huyo ataweza kurejesha makali yake, kwa sasa wanazifanyia kazi changamoto zinazomkabili
"Bado kuna kazi inafanyika tunaendelea nayo ili awe katika ubora tunaoutaka," amesema
"Alikuwa na changamoto ya kuongezeka uzito, angalau amepungua kiasi"
"Muda wa kufanyia kazi changamoto zake upo, atatakiwa tu kuweka juhudi zaidi, ili arudi kivingine na kuibeba Yanga"
Yanga inajiandaa kuikabili Zesco United kwenye mchezo wa marudiano ligi ya mabingwa ambao utapigwa Septemba 28 huko Zambia
Mabingwa hao wa kihistoria ni lazima wafunge angalau bao moja ili wawe na nafasi ya kutinga makundi