Makamu Mwenyekiti wa Yanga Fredrick Mwakalebela ataiongoza timu ya ushindi nchini Botswana kwenye mchezo wa marudiano wa ligi ya mabingwa dhidi ya Township Rollers
Mwakalebela alitangulia mapema Botswana na msafara wa viongozi wa timu hiyo kuweka mambo sawa kabla ya Yanga kuwasili
Kikosi cha Yanga kilisafiri jana kuelekea Botswana kikipitia Afrika Kusini
Makamu Bosi huyo wa Yanga amesema ameshaweka sawa mazingira yatakayowawezesha kuwashangaza Township Rollers katika mchezo huo kwa kuwafunga wakiwa kwao
"Mimi nilitangulia mapema ili kuweka kila kitu sawa kabla ya timu haijatua huku," amesema Mwakalebela
"Ninachopenda kuwaambia Wanayanga, kila mmoja atuombee, nimeshaandaa mazingira ya ushindi, kilichobaki ni dua zao tu na jitihada za wachezaji na benchi la ufundi"
Aidha kitendo cha Yanga kuwasili mapema Botswana kimewashtua Rollers ambao kocha wao Tomas Truca amesema bado mchezo huo uko wazi ingawa wao wana faida ya bao la ugenini
Matumaini ni makubwa kwa Yanga kuweza kufanya vizuri kwenye mchezo huo
Ingawa Rollers watapata sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wao, hilo haliwatishi Yanga kwani mwaka jana walicheza hapo Gaborone na kupata matokeo ya suluhu ya bila kufungana