Yanga imelazimishwa sare ya bao 1-1 na Township Rollers kwenye mchezo wa kwanza wa ligi ya mabingwa, hatua ya awali
Mchezo huo uliopigwa uwanja wa Taifa, ulishuhudiwa na mashabiki wachache waliojitokeza uwanjani kinyume na ilivyotarajiwa
Bao la mapema walilofunga Rollers kwenye dakika ya saba liliivuruga Yanga dakika hizo za mwanzo kabla ya kutulia kusaka bao la kusawazisha
Yanga ingerejea mchezoni kwenye kipindi cha kwanza kama Patrick Sibomana angeweka kambani mkwaju wa penati uliopatikana
Katika kipindi cha pili, Yanga ilikuwa bora zaidi ikitawala mchezo na kupanga mashambulizi


Hata hivyo Rollers waliokuwa wakijilinda timu nzima, waliondoa hatari zote langoni kwao
Kwenye dakika ya 86 Yanga ilipata mkwaju mwingine wa penati baada ya mlinzi wa timu hiyo kuunawa mpira ndani ya eneo la hatari
Safari hii Sibomana hakufanya makosa, akaisawazishia Yanga
Matokeo hayo ya sare bado yanaipa Yanga nafasi ya kusonga mbele kama itaweza kushinda mchezo wa ugenini
Matumaini yapo kwani Rollers wameonekana sio timu ya kutisha
Yanga ilicheza kwenye dimba la Rollers mwaka jana na haikupoteza mchezo (0-0)
Kocha Mwinyi Zahera atakuwa na wiki mbili za kukiandaa kikosi chake kabla ya mchezo huo