Baada ya kucheza pamoja kwenye mechi kadhaa, washambuliaji Juma Balinya, Patrick Sibomana na Sadney Urikhob wametengeneza utatu hatari uliopachikwa jina la BSS
Washambuliaji hao kesho wanatarajiwa kuiongoza Yanga kwenye mchezo wa ligi ya mabingwa dhidi ya Township Rollers
Katika michezo ya kirafiki ambayo Yanga imecheza, mabao mengi yamepachikwa na wakali hao
Ukiangalia takwimu za michezo mitatu iliyopita, Yanga imefunga mabao sita, manne yamefungwa na washambuliaji hao
Juzi kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Mlendege, walihitaji dakika 45 tu kupachika mabao matatu
Balinya, Sibomana na Sadney wanafahamu kuwa siku ya kesho matumaini ya Watanzania wanayanga yatakuwa mikononi mwao
Kocha Mwinyi Zahera amesema hana mashaka na uwezo wa nyota hao pamoja na wachezaji wengine wa kikosi chake
Zahera amewataka mashabiki wajitokeze kwa wingi uwanja wa Taifa kesho waje washuhudie burudani 'mbashara'
"Sina mashaka na wachezaji wangu, niwaambie tu mashabiki wetu, wasiwe na presha, waje kwa wingi uwanjani kwani watafurahi," amesema
"Msimu huu ni wa furaha kwao, wana timu nzuri sana"
Mchezo wa kesho ni wa kisasi kwa Yanga ambayo ilipoteza kwa kufungwa mabao 2-1 kwenye mchezo uliozikutanisha timu hizo mwaka jana
Β