Mabingwa wa kihistoria Tanzania Yanga leo wanaandika historia nyingine uwanja wa Taifa katika tukio la kilele cha wiki ya Mwananchi
August 04 ni siku iliyokuwa ikisubiriwa kwa hamu na mashabiki wa timu hiyo, hatimaye imewadia
Yanga leo inatambulisha kikosi chake kilichosukwa upya na kocha Mwinyi Zahera, huo ukiwa ni mwanzo wa kurejesha furaha ya mashabiki iliyopotea kwa misimu miwili
Tukio hilo litafuatiwa na mchezo wa kukata na shoka dhidi ya mabingwa wa taji la Sportpesa, Kariobangi Sharks kutoka nchini Kenya
Kutakuwa na burudani nyingi uwanja wa Taifa, kabla ya mchezo wa siku, kutakuwa na michezo miwili ya utangulizi
Katika mchezo wa kwanza, Bongofleva wakiongozwa na Ali Kiba watachuana na Bongomuvi watakaoongozwa na Vicent Kigosi 'Ray'
Mchezo wa pili utawakutanisha wakongwe wa Yanga dhidi ya wenzao wa Pamba Fc kutoka jijini Mwanza
Mageti ya uwanja wa Taifa yatafunguliwa mapema tu, saa mbili asubuhi na yatafungwa saa nane mchana
Wanayanga wameaswa kuwahi uwanjani ili kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza