Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema amepata mwamko mkubwa jana baada ya kuhudhuria hafla ya uzinduzi wa kampeni maalum ya kuichangia Yanga na kuwahakikishia Wanajangwani kuwa msimu ujao utakuwa wa furaha kwao
Akizungumza kwenye hafla hiyo iliyofanyika mkoani Dodoma, Zahera ameeleza kushangazwa na sapoti kubwa kutoka kwa wadau wa klabu ya Yanga licha ya timu hiyo kupita katika kipindi kigumu
Amesema Yanga imejidhihirisha kuwa na mashabiki wengi na amesisitiza ni wakati sasa kwa Wanayanga kuibeba timu yao wao wenyewe bila ya kusubiri tajiri mmoja
"Katika muda niliofanya kazi hapa, nimesoma na kujifunza vitu vingi sana," alsema Zahera
"Hata kwa hiki nnachoshuhudia leo hakika kimenipa hamasa sana! msimu ujao hatutoumia.
Nimetembea karibu nchi zote za Afrika nikiwa na timu ya Taifa, nawahakikishieni hakuna hata nchi moja yenye mashabiki kama hawa wa Yanga, hata TP Mazembe haina fanbase kubwa kama Yanga.
"Najiuliza kuna ulazima gani timu kama hii eti kungoja tajiri mmoja aje awekeze pesa zake?wakati wenyewe mnasema hii ni timu ya wananchi? kwanini wananchi tusiibebe timu yetu wenyewe? Sasa tunapaswa kuibeba wenyewe. . timu kama Yanga SC inapaswa kushindania makombe makubwa Afrika. Naomba tuichangie Yanga"
Zahera amewahakikisha Wanayanga kuwa msimu ujao watakuwa na kikosi imara kitakachokuwa na uwezo wa kuwania mataji makubwa barani Afrika
Amesisitiza kila mdau kuendelea kuichangia timu ili yale yote yaliyopangwa yaweze kukamilishwa kwa wakati