Kocha Msaidizi wa AS Vita Club Raoul Shungu ameomba sapoti ya mashabiki wa Yanga kuelekea mchezo wa ligi ya mabingwa ambao timu hiyo itachuana na Simba Jumamosi
Shungu amewahi kuinoa Yanga mwishoni mwa miaka ya 90 na mwanzoni mwa miaka ya 2000 akifanikiwa kutwaa taji la ubingwa wa Afrika Mashariki na Kati nchini Uganda
"Mimi sio mgeni hapa Tanzania. Nilifundisha Yanga kwa misimu mitatu," amesema Shungu katika mazoezi ya Vita Club yanayofanyika katika viwanja vya Gymkhana jijini Dar es salaam
"Marafiki zangu wa Yanga mkuje kwa wingi Jumamosi mtuunge mkono"
Vita Club hutumia jezi za kijani na njano kama ilivyo kwa Yanga hivyo kufanya baadhi ya mashabiki wa Simba kuingiza hisia kuwa timu hiyo ina 'Uyanga'
Ukiachilia mbali uwepo wa Shungu ambaye aliwahi kuwa kocha wa Yanga, Kocha Mkuu wa Vita Club ni Florent Ibenge ambaye ni rafiki mkubwa wa kocha wa Yanga Mwinyi Zahera
Ibenge pia ndiye kocha Mkuu wa timu ya Taifa ya DR Congo na alimteua Zahera kuwa msaidizi wake katika majukumu ya kukinoa kikosi cha timu hiyo
Wakati huu ambao Ibenge yuko hapa nchini, Zahera amerejea Congo kuendelea na maandalizi ya kikosi chao cha timu ya Taifa ambacho March 24 kitachuana na Liberia katika mchezo wa kusaka tiketi ya kutinga fainali za AFCON 2019