Mratibu wa Matawi ya Yanga mkoa wa Dar es salaam Kaisi Edwin amesema wamebaini kuwepo kwa baadhi ya viongozi ndani ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) ambao wanatumia nafasi zao kuivuruga Yanga
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kaisi aliwataka viongozi hao waiache Yanga ifanye mambo yake yenyewe.
Amesema wanakusudia kupeleka malalamiko yao kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dk John Magufuli kuhusu baadhi ya wateule wake ambao wanatumia nafasi zao vibaya
"TFF ijikite katika kutatua changamoto za mpira wa miguu nchini kuliko kujiingiza kwenye masuala ya vilabu," alisema Kaisi
"Mpira wetu una changamoto nyingi sana, badala ya TFF kushughulikia changamoto hizo, inajiingiza kwenye siasa za uchaguzi wa Yanga"
Kaisi amedai kuwa na ushahidi wa mmoja wa viongozi waandamizi wa TFF kuwashawishi baadhi ya viongozi wa Yanga wajiuzulu nafasi zao ili klabu hiyo ifanye uchaguzi wa nafasi zote
Hivi karibuni ziliibuka taarifa kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji, Thobias Lingalangala na Kaimu Makamu Mwenyekiti wa Yanga Siza Lyimo wamejiuzulu nafasi zao
Yanga ilipaswa kufanya uchaguzi wa kujaza nafasi zilizowazi ambazo ni Mwenyekiti, Makamu Mwenyekiti na Wajumbe wanne wa Kamati ya Utendaji
Licha ya awali kufikiwa mnakubaliano ya uchaguzi huo kufanyika March 24, huenda uchaguzi huo usifanyike kutokana na mvutano uliopo