Wabunge ambao ni mashabiki wa Yanga wameanza mikakati ya kuhakikisha timu yao inaibuka na ushindi katika mchezo wa watani wa jadi kati ya Yanga na Simba Februari 16, 2019.
Wabunge hao wamesema hayo bungeni jijini Dodoma jana wakati wakizungumza na wanahabari
Katika hatua nyingine, Mbunge wa Jimbo la Mpendae visiwani Zanzibar Mh Salim Turkey alikabidhi mipira 25 kwa Mwenyekiti wa Yanga bungeni Venas Mwamoto.
Mipira hiyo itakabidhiwa kwa kikosi cha Yanga leo kama njia mojawapo ya kujiandaa na mchezo wao dhidi ya Simba.
Wabunge hao watakuwepo dimba la Namfua wakati Yanga itakapokuwa ikichuana na Singida United katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara
Waitahadharisha TFF kuhusu ratiba
Mbunge wa Manonga, Seif Gulamali kwa niaba ya wabunge ambao ni mashabiki wa Yanga amelalamikia upangaji wa ratiba kuwa na upendeleo kwa baadhi ya timu
Gulamali amehoji hatua ya Yanga kutakiwa kurudi kucheza Tanga mara mbili ndani ya wiki moja kuwa ni dalili za hujuma
"Wanapanga ratiba ambayo si rafiki. Sasa hatuelewi kama ni hujuma ama ni kitu gani"
"Haiwezekani timu uitoe Tanga, uirudishe Singida halafu uipeleke tena Tanga"
"Bora wangefanya mechi wakacheza Tanga wakamaliza zote dhidi ya Coastal na JKT Tanzania halafu timu ikaelekea Singida, ikacheza na Singida United kisha ikarudi Dar", amesema Gulamali
"Sisi tunatoa wito kwa TFF, tunaona ratiba zao jinsi wanavyozipanga haziwi rafiki kwa timu nyingine lakini hali ikiwa tofauti kwa baadhi ya timu"
"Mfano ni kwa watani zetu Simba ambao wamecheza michezo 14 tu huku timu nyingine zikiwa zimeshuka dimbani mara 24, wana viporo 10"