Vinara wa ligi kuu ya Tanzania Bara Yanga kesho Jumatano watashuka katika uwanja wa Namfua kuikabili Singida United katika mchezo wa ligi kuu ya Tanzania Bara, mzunguuko wa 25
Yanga iliyotua mkoani Singida jana usiku, inahitaji kushinda mchezo huo ili kuendelea kujiimarisha kileleni na kujiwekea mazingira mazuri ya kutwaa ubingwa
Aidha matokeo ya sare ya bao 1-1 yaliyopatikana mkoani Tanga juzi dhidi ya Coastal Union, yanaufanya mchezo huo kuwa na umuhimu kwa Yanga kushinda
Leo jioni Yanga inatarajiwa kufanya mazoezi yake ya mwisho katika uwanja huo wa Namfua ambao utatumika kesho
Katika mchezo wa mzunguuko wa kwanza uliopigwa uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Yanga ilifanikiwa kuondoka na alama zote tatu kwa ushindi wa mabao 2-0
Mabao yote ya Yanga yalifungwa na Amissi Tambwe
Tambwe aliyekosa mchezo dhidi ya Coastal Union, hali yake imeimarika na huenda akapata nafasi ya kuiongoza safu ya ushambuliaji ya Yanga hapo kesho
Yanga iliondoka mkoani Tanga ikiwa na kikosi chake kamili na inatarajiwa kurejea tena mkoani humo baada ya mchezo wa kesho kwa ajili ya kwenda kuwakabili JKT Tanzania katika mchezo ambao utapigwa Februari 09
Mtiririko wa ratiba hii umewashangaza wengi kwani wakati huu ambao ligi haina mdhamini, ilidhaniwa ratiba ilipaswa kuzingatia kuzipunguzia timu gharama
Yanga ingeweza kucheza na Singida United kwanza kisha kuelekea mkoani Tanga kumalizia michezo miwili dhidi ya Coastal Union na JKT Tanzania
Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amesema ingawa ratiba sio rafiki kwa timu yake, lakini wanahitaji kupambamba kuhakikisha wanapata matokeo ili wasiharibu lengo la kutwaa ubingwa msimu huu