Kocha Mkuu wa Yanga Mwinyi Zahera amefichua kuwa kabla ya kuja nchini kujiunga na mabingwa hao wa kihistoria, ilikuwa ajiunge na Buildcon inayoshiriki ligi kuu ya Zambia.
Akihojiwa katika kipindi cha Nyundo ya Baruani, Zahera amesema alifika Zambia na kufanya kazi katika klabu ya BuildCon kwa takribani wiki moja kabla ya kuondoka kuja nchini.
Zahera amesema mdogo wake alichangia kwa kiasi kikubwa kumleta Tanzania licha ya kukiri lugha ya kiingereza pia ilikuwa changamoto kwake katika kutekeleza majukumu yake kwa kuwa yeye anazungumza Kifaransa.
"Nilikwenda Zambia kujiunga na klabu ya BuildCon. Nilifanya kazi pale kwa siku chache kabla mdogo wangu kunipigia simu nije Tanzania kujiunga na Yanga"
"Aliniambia Yanga ni timu kubwa Afrika na baada ya kutua nchini na kufanya kazi na Yanga nimeamini kwani nimeuona ukubwa wa Yanga," alisema Zahera
Zahera amefichua kuwa siku aliyoondoka Zambia ndio siku ambayo ilikuwa asaini mkataba wa kuitumikia Buildcon aliyoisaidia kushinda michezo miwili na kutoka sare mchezo mmoja dhidi ya Nkana Fc. Kabla ya yeye kuwasili timu hiyo iliyokuwa ikinolewa na makocha kutoka Italia ilikuwa imefungwa michezo minne mfululizo.
Zahera amesema licha ya changamoto zinazoikabili Yanga, yeye ameridhika kuwa sehemu ya wanafamilia wa Yanga kwa kuwa hakufuata fedha katika klabu hiyo.
Zahera amesema anaamini Yanga inapita katika kipindi cha mpito tu wakati utafika timu hiyo itarudi katika nyakati zake kama zamani