Mabingwa wa kihistoria wa Tanzania Yanga wameendelea kuchanja mbuga kileleni mwa msimamo wa ligi baada ya leo kuiaza Mbeya City mabao 2-1 katika mchezo mkali uliopigwa dimba la Sokoine.
Alikuwa ni Mcongoman Heritier Makambo aliyeihakikishia Yanga alama tatu muhimu baada ya kufunga mabao yote mawili kwenye mchezo huo.

Bao la kwanza alilifunga katika dakika ya 17 akiunganisha mpira wa adhabu uliopigwa na Ibrahim Ajib ambaye ameendeleza 'moto' wake wa kuipikia Yanga mabao.
Mbeya City walisawazisha bao hilo kupitia kwa Iddi Selemani kabla Makambo hajatumbukiza kambani bao la pili kwenye dakika ya 41 akiunganisha kwa kichwa krosi ya Paulo Godfrey 'Boxer'
Licha ya Mbeya City kutoa upinzani mkali kwa vinara hao wa ligi, lakini mpaka dakika 90 za mchezo huo zinakamilika, Yanga iliweza kushinda mchezo wa 16 kati 18 na kufikisha alama 50
Matokeo hayo pia yanamaanisha Yanga ndio timu pekee ambayo haijapoteza mchezo kwenye ligi baada ya Azam Fc kufumuliwa mabao 2-0 na Mtibwa Sugar huko Manungu.
Nae Makambo ameshika usukani wa vinara wa ufungaji baada ya leo kufikisha mabao 11 na kuwaacha nyuma Eliud Ambokile na Said Dilunga wakiwa na mabao tisa.
Yanga inaongoza ligi kwa tofauti ya alama 10 dhidi ya Azam Fc inayoshika nafasi ya pili ikiwa na alama 40.